Dk. Kigwangalla: “CHF iliyoboreshwa ni nguzo imara kwenye mkakati wetu wa Bima ya Afya”

Dk. Kigwangalla: “CHF iliyoboreshwa ni nguzo imara kwenye mkakati wetu wa Bima ya Afya”

CHF iliyoboreshwa itakuwa nguzo imara kwenye mkakati wetu wa kuelekea kwenye bima ya afya ya lazima kwa watu wote. Kwa sasa tuna miradi kwenye mikoa tisa. Miradi hii inatekelezwa na washirika wetu mbalimbali.

“Sisi kama Wizara ya Afya tutaanza na mikoa mitatu wakati ili kujifunza kabla hatujatanuka na kumalizia mikoa yote ya Tanzania bara. Pamoja na mikoa hiyo tisa, ambapo kuna miradi ya wabia na washirika wetu wa maendeleo, tutafikisha mikoa 12, itabaki mikoa 14. Hii itasubiri ridhaa ya ngazi mbalimbali za maamuzi ndani ya serikali kupima uwezo wetu”.

Hata hivyo, tayari mimi na kikosi kazi changu tulikwishafanyia kazi mpango wa muda mfupi wa  maboresho ya mfuko wa afya ya jamii (CHF), na tayari tumeandaa mapendekezo ya muswada wa Sheria ya Bima ya Afya ya Lazima kwa Wote.

CHF iliyoboreshwa ni kitu tofauti sana na CHF iliyopo sasa. Main features zake ni kama ifuatavyo: –

 CHF iliyoboreshwa inakuja na mkakati wa kiufundi ambapo tunabadili kabisa muundo wa kiutawala wa fedha na malipo ya watoa huduma kwa kumtenganisha ‘provider’ wa huduma (mtoa huduma) na ‘purchaser’ wa huduma (mlipia/mnunua huduma). Hii ni principle muhimu kwenye mifumo ya bima. kwa maana hiyo basi, CHF iliyoboreshwa inaenda kuwa kama ‘bima ya kijamii’ fulani hivi.

CHF iliyoboreshwa itakuwa na mchango mkubwa kidogo kuliko ya sasa, kwa sababu itamuwezesha mmiliki wa kadi ya CHF iliyoboreshwa kuwa na fursa ya kupata huduma kutokea ngazi ya zahanati kijijini kwake, kijiji cha jirani ndani na nje ya wilaya yake, lakini mkoani humo humo – kwa maana nyingine ni kwamba CHF iliyoboreshwa itampa fursa mmiliki wa kadi hiyo kupata huduma kutoka ngazi ya zahanati kijijini mpaka hospitali ya rufaa ya mkoa.

Matumaini yetu ni kuwa, kama mwananchi mwenye kadi ataweza kupata huduma za msingi mpaka huduma za rufaa mkoani atakuwa amepunguziwa adha kubwa sana ya kufuata matibabu ya uhakika mbali.

Mpango huu utaenda sambamba na azma yetu ya kubadili muundo wa kutoa huduma za afya kwa kutenganisha umiliki na uendeshaji wa vituo kama ifuatavyo; kwamba, Mfumo wa Afya ya Msingi (Primary Healthcare) uanzie ngazi ya kaya na jamii (ambapo tunaweka utaratibu wa wahudumu wa afya vijijini), Zahanati, Kituo cha afya (yaani Health Center) mpaka ngazi ya Hospitali ya wilaya, na kwa upande wa pili, mfumo wa huduma za rufaa (referral services) uanzie ngazi ya Hospitali ya Rufaa ya Mkoa, Kanda, Taifa na Hospitali zenye kutoa huduma maalum.

 Kadi ya CHF iliyoboreshwa itakuwa ya kielektroniki na itasomeka mkoani pote, itapatikana kwa urahisi zaidi kuliko ilivyo sasa.

Uchangiaji kwenye CHF iliyoboreshwa utabaki kuwa wa hiari kama sheria zinavyotaka.

Makundi maalum yanayopewa msamaha kwa mujibu wa sera ya afya ya taifa yatahudumiwa na halmashauri husika kutokana na mapato ya ndani kama ambavyo sheria ya CHF inaelekeza. Wananchi kwenye vijiji watalazimika kuwabaini wanaopaswa kupewa msamaha huu wa kutochangia CHF iliyoboreshwa kwa kuwa wao wanajuana kuwa ni nani kweli hana uwezo na nani anadanganya ili walengwa tu ndiyo wafaidike na kulipiwa michango na serikali.

Gharama za kupata huduma kwenye vituo vya serikali zitaongezeka kidogo kwa sababu CHF iliyoboreshwa inapaswa kuja pamoja na huduma bora za afya, na huduma bora haziwezi kutolewa bila uwepo wa makusanyo ya pesa za kutolea huduma.

 Kamati za Vituo zitawajibika kushiriki kikamilifu kwenye upokeaji wa dawa, udhibiti wa matumizi yake na uendeshaji wa vituo. Tutaimarisha ukaguzi ili kuhakikisha bajeti kubwa ya dawa iliyowekwa na serikali kwenye mwaka huu wa fedha inaenda ku-reflect kwenye upatikanaji wa uhakika wa dawa, vifaa, vifaa tiba na vitendanishi. Kamati za Afya zitasimamia uwepo wa uwazi wa matumizi ya fedha za kituo na madawa, vifaa, vifaa tiba na vitendanishi vinavyonunuliwa na vinavyoletwa kwa ruzuku ya serikali kuu.